Ukiangalia katika agano jipya jinsi Mungu alivyowachukulia wale wote waliokuwa wanamlalamikia tunaona kuwa kwa Mungu tendo la kulalamika lilikuwa ni sawa na watu kuonyesha kuwa hawana imani naye. Walipolalamika kuhusu maisha wanayoishi, chakula wanachokula na hata uongozi wa Musa, Mungu hakufurahishwa nao sababu walionyesha kuwa hawana shukrani na yale ambayo amewatendea na kuwatoa utumwani katika nchi ya Misri.
Alikasirishwa na jinsi walivyokosa imani kwake kwamba anaweza kuwalinda, kuwapa mahitaji yao na kuwaongoza hadi kufika nchi ya ahadi. Hesabu 11:1 Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. Kulalamika ni ishara ya kutokuamini Haijalishi ni hali gani imepelekea wewe kutokuridhika, kulalamika mara zote huonyesha kukosa imani kuwa Mungu anaweza kuyaongoza maisha yako.
Unapoamua kumpa Yesu maisha yako ina maana unamfanya yeye awe kiongozi wa maisha yako, sasa pale unapolalamika na kunungu’unika ina maana unaonyesha kuwa yeye ameshindwa kukuongoza, yeye ambaye umempa uongozi wa maisha yako. Kutoka 16:8b kwa kuwa BWANA asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia yeye; na sisi tu nani? manung’uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA. Kulalamika ni kutokuliamini neno la Mungu ambalo linasema kuwa Mungu hufanya mambo yote kwa ajili ya kutupatia mema, ukitambua neno hili hautaweza kulalamika bali utamshukuru Mungu kwa mipango yake ambayo ni kwa ajili ya kutupatia mema.
Warumi 8:28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Haata pale ambapo unaona mambo yamekuwa magumu na huwezi kuendelea, usimpe ibilisi nafasi ya kukutoa kwenye mpango wa Mungu kwa kuanza kulalamika, bali wewe mshukuru Mungu na endelea kuamini mpango wake katika maisha yako kuwan i kamili na atautimiliza.
Katika mambo yote mshukuru Mungu maana ni mapenzi yake katika Kristo Yesu. Kulalamika kunampa shetani nafasi Kulalamika kunafungua milango katika maisha yetu na kutoa nafasi kwa shetani kuharibu, shetani hupenda watu wanaolalamika na hutumia nafasi hiyo kujaza chuki na kiburi katika mioyo yao. Wana wa Israeli walipolalamika matokeo yake waliangamizwa kwa sababu kulalamika kuliwapa kiburi na kumdharau Musa na kisha kutengeneza sanamu na kuziabudu.
1Korintho 10:10 Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharibu. Pia kulalamika kunamkashirisha Mungu na anakuwa mbali na mtu anayelalamika na katika hali hiyo shetani anapata nafasi ya kuingia na kuharibu. Kulalamika sio sifa ya mkristo Wafilipi 2:14 Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano.
Yuda 1:15-16 inaonyesha kuwa watu wenye kulalamika ni sawa na watu waovu wasioamini, waendao kwa tamaa zao. Mtu anayemjua Mungu amejaa imani na mwenye moyo wa shukrani mara zote akiyatazama yale mazuri na kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Kulalamika ni ishara ya kutolitii neno la Mungu. Kulalamika hakubadilishi hali iliyopo bali kunaongeza maumivu na uchungu ndani ya yule anayelelamika. Ni vyema tukaichunga mioyo yetu ili tusije ingia kwenye dhambi hii ya kulalamika.
No Comments Yet...