Kwa wasichana mabinti wa kristo, napenda leo tujifunze umuhimu wa kujitambua.
Ni lazima ujitambue nafasi yako na umuhimu wako ndani ya kanisa na jamii kwa ujumla. Kuna mambo machache ambayo ni vizuri tukielimushana na kufundishana.
1. Jitambuwe wewe ni wa thamani Umenunuliwa kwa gharama kubwa ambayo ni damu ya Yesu. Thamani yako ni kubwa sana ukilinganisha na mabinti wasiomjua Mungu. Usipojitambua hutawezi kujithamini wala kujitunza. Mtu anapotambua thamani ya kitu ndipo anapokuwa na bidii ya kukitunza, ukitambua thamani yako utajitunza kwa gharama yoyote na kwa bidii.Umechaguliwa miongoni mwa wengi, tafakari Mungu alipokutoa na ufahamu kuwa unathamani sana mbele zake.
2. Jiheshimu na Kujithamini Ukitaka watu wanaokuzunguka wakuheshimu basi inabidi wewe kwanza ujiheshimu. Binti yeyote aliyeokoka yampasa awe anajiheshimu sana. Angalia unavyoenenda katika maisha yako ya kila siku, unavyoongea na watu mbalimbali, unavyovaa na hata unavyohudumu katika nyumba ya Bwana. Ukiona mtu haheshimiwi na watu ukichunguza utakuta yeye mwenyewe hajiheshimu. Usiruhusu utani uliovuka mipaka hasa na watu wa jinsia tofauti maana ni rahisi kushuka kwa heshima yako. Uwe ni mtu mwenye mipaka katika kila jambo (kiasi).
3. Jitunze Ukishatambua thamani yako itakuwa rahisi kwako kujitunza. Kitu muhimu cha kwanza ni kuutunza wokovu wako kwa kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu. Kisha hakikisha unatunza pia na maisha yako na mwili wako pia ambao ni hekalu la roho mtakatifu. Uwe msafi, nadhifu (kuwa nadhifu haimaanishi kuwa na hela nyingi) na hakikisha mara zote upo katika muonekano mzuri. Wewe kama msichana ni lazima ujipende wakati wote. Pia tunza usichana wako usichezewe na mtu yeyote, uwe na msimamo thabiti na kila mtu afahamu hilo.
4. Jishughulishe Kuna wasichana wengine wanaridhika kukaa kwa wazazi na kufanyiwa kila kitu. Kama nyumbani kuna msaidizi basi ndio hata jikoni haingii, hii haifai kwa msichana aliye okoka. Ni vizuri uka wa mchapakazi hata kama unasoma au umeajiriwa. Hakikisha kazi zote za nyumbani unaziweza tena kwa ufasaha. Pia ni vizuri kufanya kazi za kuingiza kipato, sio lazi ma uwe umeajiriwa unaweza ukajiajiri mwenyewe na kupata mafanikio makubwa. Usibweteke na kusubiri kuwa ukiolewa mume atakupa kila kitu, nivizuri ukiwa na tabia ya kufanya kazi na kupenda kufanya kazi.
5. Omba Maombi ndio jambo la muhimu sana, hutaweza kufanya hayo yote bila kupata uongozi na msaada wa Mungu. Ni lazima uwe na muda wa kuzungumza na Mungu binafsi na pia kusoma neno lake. Maombi yanavunja nira na kuondoa vikwazo vyote na ni lazima yawe sehemu ya maisha yako kama unataka kuona nguvu za Mungu katika maisha yako.
No Comments Yet...