ZABURI:- UCHAMBUZI NA UFAFANUZI Bwana Yesu asifiwe. Karibu tujifunze pamoja na kukichambua kitabu cha Zaburi. Kitabu cha Zaburi ni mkusanyiko wa mawazo ya rohoni kuhusu mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu. Maneno ya mwimba zaburi ni lugha ya moyo wa mwamini, either kuhuzunika kwa sababu ya dhambi, au kuonyesha kiu yake kwa Mungu, au kufurahia jambo la kiMungu.
Pia kupitia kitabu cha Zaburi tunaona mioyo iliyougua kwa sababu ya mapito magumu na mateso, fikra za watu walioshindana sana na majaribu, furaha ya watu walioshangilia ukombozi, na shangwe ya watu waliomwabudu Mungu kinabii kwa kutabiri ujio wa Kristo miaka mingi mbeleni. Mtheolojia Matthew Henry kupitia kitabu chake bora kiitwacho Matthew Henry’s Bible Commentary anasema, ikiwa tutauelewa ujumbe wa Kitabu cha Zaburi na kuutendea kazi, chochote tutakachoomba kutoka kwenye kiti cha rehema kwa sala na maombi, kwa neema tutapewa. Kitabu cha Zaburi kiliandikwa ili kisomwe kwa kuimba kwa kufuatana na ala za muziki; anasema Mtheolojia Don Fleming na kuongeza kwamba, msomaji halazimiki kusoma sura za kitabu hiki kwa mfuatano kwani kila sura imebeba wazo la kipekee kuhusu kusifu na kumwabudu Mungu. Nani mwandishi wa kitabu cha Zaburi? Wapo waandishi wengi walioshiriki kuandika kitabu cha Zaburi.
Na hao waandishi hawakuwa pamoja, waliishi duniani nyakati tofauti. Mwandishi nguli wa vitabu vya kiroho M. G. Easton katika kitabu chake kiitwacho Easton’s Bible dictionary anadai kwamba kazi ya kuandika sura zote za kitabu cha Zaburi ilifanyika kwa karibia miaka 1000 tangu mwandishi wa kwanza hadi wa mwisho. Mara nyingi sura za kitabu cha Zaburi huanza kwa kumtambulisha mwandishi. Tukisoma 1 Sam 16:23; 2 Sam 1:17-27; 23:1 tunaona wazi kwamba Mfalme Daudi alibarikiwa kipawa cha Muziki na Ushairi (He was a gifted musician and poet).
Mfalme Daudi ndiye muasisi wa mpangilio wa waimbaji katika ibada za hekaluni pale Yerusalemu, kulingana na 1 Nya 15:16-28; 16:7. Waimbaji na wanamuziki waliohudumu hekaluni walijulikana kama Walawi. Mfalme Daudi aliwapanga na kuwagawa katika makundi matatu kulingana na majina ya wana wa Lawi, yaani Gershon, Kohathi na Merari. Unaweza kusoma Zaidi habari za Mpangilio wa hizi kwaya tatu hekaluni; 1 Nya 6:1,31-48; 15:19; 2 Nya 5:12. Gershon, yaani Kundi la kwanza la Waimbaji liliongozwa na Asafu. Asafu anajulikana kama mwandishi wa sura 12 za kitabu cha Zaburi (Zab 50; 73-83). Asafu alikuwa nabii (2 Nya 29:30), Kohathi, yaani kundi la pili la waimbaji liliongozwa na Hemani. Hemani ndiye mwandishi wa Zaburi 88. Merari, yaani Kundi la tatu la Waimbaji liliongozwa na Ethani (Yeduthuni). Ethani ndiye mwandishi wa Zaburi ya 89. Hemani na Ethani walikuwa na hekima ya kipekee sana (1 Fal 4:31). Mfalme Sulemani ndiye mwandishi wa sura mbili, yaani Zaburi 72, na 127. Zaburi ya 90 imeandikwa na Nabii Musa., na inasadikika ndiyo sura ya kitabu cha Zaburi iliyoandikwa zamani Zaidi.
Kitabu cha Zaburi ni ushairi unaozingatia Zaidi lugha, desturi, tabia na tamaduni za Wayahudi. Ladha ya vina na mizani katika ushairi wa Kiebrania vimekipamba sana kitabu hiki cha Zaburi. Mshairi huleta wazo la msingi kwa kusema sentensi mbili zinazoshabihiana (two parallel statements), ambapo sentensi ya pili hurudia wazo la sentensi ya kwanza kwa maneno tofauti kidogo. Mfano Zaburi 27:1; 104:28,33 Wakati mwingine mshairi hujaribu kubalance wazo kwa kutumia sentensi mbili, ambapo sentensi ya kwanza huonyesha ukweli na sentensi ya pili huonyesha kinyume chake, mfano Zab 37:9 Wakati mwingine katika Zaburi Mshairi hutumia sentesi ya kwanza kuonyesha ukweli fulani na sentensi ya pili kuonyesha matumizi ya huo ukweli, mfano Zab 103:5,13 .
Ziko sura zinazoitwa “Messianic Psalms”, yaani Zaburi zilizotabiri mambo mbali mbali kuhusu Yesu Kristo, kuzaliwa kwake, maisha na wito wake, kufa na kufufuka kwake, uungu na umilele wake, neema na rehema zake, utukufu wake na mengineyo. Msoma Zaburi akishindwa kumwona Yesu ndani ya Kitabu cha Zaburi atakuwa ameshindwa kuelewa ujumbe mkuu wa Biblia na hasa kitabu hiki kitamu cha Zaburi. Biblia ina sura 1189. Zaburi 118 ndiyo chapter ambayo ni ya kati kati katika Biblia. Na kama tungehesabu mistari yote ya Biblia, mstari ulio katikati ya Biblia (inasemekana) ni Zaburi 118:8.
Huu ndio mstari ambao inasadikika ni mstari uliobeba ujumbe wa msingi wa Biblia yote. It is the center of the Bible. Kama ni kweli mstari huu ndio senta ya Biblia, unasema nini cha pekee? Tuutazame, mstari huo unasema, “Ni heri Kumkimbilia Bwana, kuliko kuwatumainia wanadamu” Hivyo tu. Ni hivyo. Mtheolojia Matthew Henry katika kuchambua maudhui ya Zaburi 118, ameigawa katika makundi mawili. Anasema ujumbe mkuu uliobebwa katika mstari 1-18 ni KUHUSU UBORA NA UMUHIMU WA MWANADAMU KUMTEGEMEA MUNGU.
Maneno hayo ya Mfalme Daudi aliyatamka baada ya kushinda na kuingia ikulu na kukabidhiwa kiti cha Ufalme wa Dola ya Israeli. Ikumbukwe kwamba Sauli alitaka kumwangamiza Daudi kwa miaka minne mfululizo (1018-1014KK). Daudi alihangaika nyikani akilala mapangoni kumkwepa mfalme Sauli. Hatimaye Daudi ameingia Ikulu. Ameketi kwenye kiti cha Ufalme. Anaitazama mikono na miguu yenye makovu. Anatafakari mara ngapi ameponea chupu chupu kuuawa na Sauli au askari wake.
Moyo wake unajawa na shukrani kwa Mungu anaanza kumwadhimisha Bwana kwa maneno ya kipekee. Anza kusoma Zab 118 kuanzia mstari wa 2 utaona Daudi anahitimisha kwa kusema, ana heri yule anayemkimbilia BWANA. Katika mistari inayofuata, Daudi anaendelea kusema maneno haya 10 Mataifa yote walinizunguka; Kwa Jina la Bwana naliwakatilia mbali 11 Walinizunguka, naam, walinizunguka, Kwa Jina la Bwana naliwakatilia mbali 12 Walinizunguka kama nyuki, walizimika kama moto wa miibani; Kwa Jina la Bwana naliwakatilia mbali 13 Ulinisukuma sana ili nianguke; LAKINI BWANA AKANISAIDIA Ndugu mpendwa na rafiki, sijui unapita wapi wakati unapousoma ujumbe huu. Lakini nakusihi uupokee ujumbe huu kutoka kwenye moyo wa Biblia (from the center of the Bible), kwamba wana heri wale walioamua kumtumaini Bwana.
Inawezekana umezungukwa na maadui kama asemavyo Daudi, kwamba walimzunguka kama nyuki, LAKINI BWANA AKAMSAIDIA, na maadui wakazimika kama moto wa miibani, ninakuombea neema ya kuinuka na kumtumaini Bwana tena, ili ushuhudie tena maadui zako wakizimwa kama moto wa miibani. Nikwambie kitu? Kuna faraja iliyosalia. Walikusukuma sana ili uanguke, lakini kwa msaada wa Mungu hutaanguka. Hutaanguka kiroho au kibiashara Hutaanguka kimasomo au kiuchumi. Daka hili na usije ukasahau hata siku moja. Ni heri Kumtumaini Bwana, kuliko kuwatumainia Wakuu. Nitafurahi kusikia ushuhuda wako, namna ujumbe huu ulivyogusa maisha yako.
No Comments Yet...